An English version of this blogpost is available here.
Kuna pengo la kiuelewa kuhusu uhusiano kati ya cheo cha mwanaume kijamii na mafanikio yake katika uzazi. Hii ni kwa mujibu wa utafiti nilioufanya na mwenzangu, miongoni mwa wanyama. Utafiti huu unaonyesha kuwa mfumo wa kijamii na kujamiiana wa fisi wenye madoadoa unaweza kutoa mwanga katika kuelewa mienendo ya usawa wa uzazi miongoni mwa jamii za mamalia.
Katika jamii nyingi za wanyama, rasilimali hazigawiwi kwa usawa miongoni mwa kikundi. Wale walio katika ngazi ya juu ya uongozi wa kijamii hula chakula kitamu zaidi, hupata sehemu za kulala zenye starehe, na wanaweza kupata wenzi wanaovutia zaidi.
Katika ulimwengu wa wanyama, ambapo mafanikio ya maisha huamuliwa kwa kiasi kikubwa na idadi ya watoto ambao mnyama huacha nyuma, ni wazi kwa nini bidii hufanyika ili kufikia kilele na kubaki huko kwa muda mrefu iwezekanavyo.
Jambo ambalo bado hatuelewi kabisa ni jinsi cheo cha kijamii kinavyoathiri mafanikio ya uzazi. Je, madume wa vyeo vya juu huzaa watoto zaidi na watoto wenye ubora wa juu kwa sababu wana nguvu na kuvutia zaidi? Au ni kwa sababu hawana wasiwasi wowote kwenye ushindani na madume wengine na wana uwezo wa kuwapata majike zaidi?
Ili kujibu maswali haya, tulifanya utafiti nyikani katika savanna ya Kiafrika. Kwa zaidi ya miaka 20 – na karibu miezi 20 ya Shahada yangu ya Uzamivu tulijikita katika kutafuta, kutambua, kutathmini uzao, na kufuatilia tabia ya maelfu ya fisi walio na madoadoa kutoka kwa koo nane za utafiti katika Bonde la Ngorongoro Kaskazini mwa Tanzania.
Pia ia tulikusanya zaidi ya vinyesi 400 vya fisi ili kupima mkusanyiko wa vichocheo vya cortisol na kukadiria, kifisiolojia, kuwa fisi hao wanapata mfadhaiko au msongo wa mawazo kiasi gani.
Tulipata ushahidi wa wazi kwamba mwingiliano na madume wengine huwa na mfadhaiko zaidi kwa madume wa vyeo vya chini kuliko wapinzani wao wa vyeo vya juu na kwamba hii inaathiri nguvu wanazoweza kuwekeza katika kuwachumbia majike waliojaaliwa na wanaoshindaniwa zaidi.
Pia tuligundua kuwa madume wanapaswa kuchanganua mapenzi na majukumu ya kawaida zaidi kama kufahamiana na wenzi wapya wa koo na kudumisha urafiki wa zamani na ushirikiano wa kimkakati. Lakini madume wa vyeo vya chini huepuka shughuli zenye kuwasababishia msongo wa mawazo na kutumia muda zaidi wakiwa peke yao, kumeza mifupa au kutulia kwenye madimbwi yenye uvundo.
Madume wa ngazi ya juu, kwa upande mwingine, wanahitaji muda mdogo wao kuwa wenyewe ili kuondoa msongo, na wanaweza kuwekeza mengi zaidi katika kukuza uhusiano wa kirafiki na majike. Na hilo ndilo jambo ambalo fisi jike hupenda zaidi.

Pia, tuligundua falsafa za madume wale ambao hupendelea kukaa nyumbani au wale “wavulana wa mama” –hawa hutoa kipaumbele kwa maswala ya uzazi badala ya kukuza mahusiano ya kijamii, na kuzingatia juhudi zao za uzazi kwa majike wenye ubora wa juu – matokeo yake hujikuta wakiwa katika nafasi ya juu kijamii ikilinganishwa na wahamiaji.
Awali, tuligundua kuwa madume wa falsafa huzaliana mapema kuliko wahamiaji na kuzaa watoto karibu na majike wa daraja la juu pekee na matokeo yasasa yanaweza kulingamishwa na hayo ya awali katika kuelewa jinsi wanaume wanavyotofautiana.
Tofauti na spishi nyingi ambapo madume hutumia nguvu zao za kimwili, pembe ndefu na meno makali ili kuwazuia wapinzani – au hata kuwalazimisha ngono majike – fisi dume wenye madoadoa hawashiriki katika mapigano makali ili kufika kileleni mwa uongozi na kuzaliana. Kwa nini basi madume wa vyeo vya chini wana msongo wa mawazo zaidi kuliko madume wa vyeo vya juu?
Fisi dume wanaweza wasiwe wanyama wakali lakini pia si wanyama wenye kupenda amani. Katika utafiti wa hivi karibuni tulionyesha kuwa uhusiano wa kiukutawala katika jamii ya fisi kimsingi hutegemea ni washirika wangapi wa kijamii ambao fisi anaweza kutegemea anapokuwa katika mzozo na wengine.
Madume wa ngazi ya chini kwa kawaida ni wageni na hawana ushirikiano wenye nguvu. Pia wako hatarini zaidi kutumiwa na wengine kama mbuzi wa kafara na hii inaweza kuwa chanzo kikuu msongo wa mawazo au mfadhaiko.
Unyanyasaji hutokea mara kwa mara miongoni mwa fisi (na wanyama wengine) na inaelekea hutumika kama njia ya kupunguza msongo au kukabiliana na mafadhaiko kisaikolojia.
Mara nyingi fisi huchukua mfumo wa msururu wa utawala ambapo madume yanayofuatana huelekeza tena uchokozi hadi kwa dume mwingine wa ngazi ya chini. Na wakati dume wa cheo cha chini kabisa kwenye mnyororo kama huo hana mnyonge wake, kukimbilia kwa mbweha asiye na hatia, mwamba, au hata gari letu la utafiti.
Lakini usiwaonee huruma madume wa chini. Wakati wao utafika.
Cheo cha kijamii cha fisi dume wenye madoadoa huamuliwa na mkusanyiko wa kupanga foleni. Madume wengi hatimaye hupanda ngazi ya kijamii na kupata kufurahia manufaa ya kuwa katika nafasi ya juu kijamii.
Inafurahisha sana kuona kwamba hata katika jamii ambapo mahusiano ya utawala yanarasimishwa na mifumo yakijamii, mwingiliano kati ya madume unaweza kuwa na athari kifiziolojia kitu ambacho kinaweza kushinikiza marekebisho ya kitabia yenye athdari (ya gharama) kiuzazi.
Utafiti wetu unarekebisha uelewa wetu kuhusu jinsi cheo cha kijamii kinavyohusiana na msongo wa mawazo na jinsi ushindani wa wanaume unavyoathiri fiziolojia, ujamaa na uimara. Pia unatoa mtazamo mpya juu ya utaratibu wakifisiolojia unaoweza kuibua mikakati mbadala ya uzazi na kuzaliana.
Makala haya yametafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza na Deusdedity Masemba, kwaajili ya kuchapishwa katika gazeti la ‘MwanaSayansi’. MwanaSayansi ni gazeti la kwanza la Sayansi kwa Kiswahili nchini Tanzania na chanzo mahususi cha habari, maoni & uchambuzi kuhusu sayansi & teknolojia.

2 thoughts on “Na Eve Davidian: Hadithi ya mapenzi, msongo na kinyesi cha fisi Ngorongoro”